Maboresho ya sheria za Tanzania kuhusu mapatano ya washukiwa kabla ya hukumu mahakamani

 MagufuliJe? sheria za Tanzania zinaruhusu washukiwa kujadiliana na mwendesha mashtaka na kufikia makubaliano nje ya mahakama na kesi kufutwa?
Kimsingi, hilo ndilo swali Watanzania wengi wamekuwa wakiulizana ama kujadiliana kwenye mitandao ya kijamii toka Rais John Magufuli alipotangaza 'ushauri' wake kwa wale wanaoshitakiwa na makosa ya uhujumu uchumi nchini humo.
Siku ya Jumapili, akiwa Ikulu jijini Dar es Salaam, Magufuli alimwagiza Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Biswalo Maganga kuwasikiliza mahabusu wanaoshtakiwa kwa kesi za uhujumu uchumi, wale wataokiri, kuomba radhi na kukubali kurudisha fedha wanazodaiwa wasamehewe.
"Najua wanateseka. Unaona wanavyopelekwa mahakamani, wengine wamekonda kweli, inatia huruma na inaumiza. Najua wengine wanataka kuomba msamaha...wale ambao watakaoshindwa kuomba msamaha, waendelee kubanwa hata kama kesi zao zitachukua miaka 20."

Maboresho ya sheria

Septemba 5 mwaka huu, Bunge la Tanzania lilipitisha muswada wa maboresho ya sheria mbalimali ikiwemo Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ambapo mapatano baina ya watuhumiwa na mwendesha mashtaka (plea bargain) yalipitishwa.
Kwa mabadiliko hayo yeyote kati ya mtuhumiwa, wakili wake ama mwendesha mashtaka anaweza kuanzisha mapatano hayo kwa kuiarifu mahakama. Mahakama kwa upande wake haitahusika na makubaliano hayo.
Katika makubaliano hayo, mshukiwa anaweza kukiri tuhuma ama sehemu ya tuhuma dhidi yake ili kupata afueni fulani ikiwemo kuondolewa baadhi ya mashtaka,ama kupunguziwa muda ama aina ya adhabu.
Mabadiliko hayo ya sheria pia yanabainisha kuwa mtuhumiwa anaweza kutakiwa kulipa fidia ama kurejesha fedha ambazo zinahusishwa na kesi anayoshitakiwa nayo.
Kwa mujibu wa muswada huo, makubaliano hayo yakishafikiwa yatapelekwa mahakamani na kutambuliwa rasmi, na mahakama awali itajiridhisha kuwa hayakuingiwa kwa kushurutishwa.
Pia mshukiwa atatakiwa kula kiapo cha kukubaliana na makubaiano hayo, pia atasomewa haki zake ikiwemo kumuondoshea haki ya kukata rufaa, isipokuwa kuhusu urefu ama uhalali wa hukumu atakayopatiwa.
Makubaliano hayo kwa mujibu wa muswada hayatafanyika kwa watuhumiwa wa makosa yafuatayo: "makosa ya udhalilishaji wa kingono ambayo adhabu yake inazidi kifungo cha miaka mitano ama inahusisha wahanga wa chini ya miaka 18, uhaini, kumiliki ama kusafirisha dawa za kulevya ambazo thamani yake ni zaidi ya milioni 10, ugaidi, kukutwa na nyara za serikali ambazo thamani yake ni zaidi ya milioni 10 bila kibali maalaumu cha maandishi cha DPP."
Muswada huo, kwa mujibu wa utaratibu, kama ilivyo kwa miswada mingine, baada ya kupitishwa bungeni utatakiwa kusainiwa kuwa sheria na raisi wa Tanzania.

Utaratibu wa msamaha kwa kesi zilizopo


Erick Kabendera
Image captionMwanahabari Erick Kabendera anashtakiwa kwa tuhuma za kukwepa kodi na kutakatisha fedha

Hii leo, DPP Maganga ameeleza utaratibu ambao utatumika na kusema ofisi yake ipo tayari kutekeleza ushauri wa Rais John Magufuli aliyetaka kusikilizwa kwa mahabusu wanaokabiliwa na makosa ya uhujumu uchumi iwapo watakuwa tayari kukiri na kurejesha fedha za serikali wasamehewe.
Mganga amesema jambo hilo linawezekana endapo mshtakiwa mwenyewe ataiandikia ofisi yake barua kupitia kwa mkuu wa gereza na kusisitiza kuwa barua hiyo inapaswa kuandikwa na mtuhumiwa mwenyewe aliye gerezani na siyo wakili.
"Utaratibu ni kwamba, mtuhumiwa mwenyewe aliyeko mahabusu anatakiwa aniandikie barua kupitia kwa mkuu wa gereza, akiri kosa na kuomba kutubu haraka iwezekanavyo na sisi tutachukua hatua."
Watu kadhaa mashuhuri kwa sasa wanakabiliwa na makosa ya uhujumu uchumi ikiwemo mwanahabari wa uchunguzi Erick Kabendera.
Mwanahabari huyo anatuhumiwa na kujihusisha na genge la uhalifu na uhujumu wa uchumi nchini Tanzania, shtaka la pili ni la kukwepa kulipa kodi ya zaidi ya milioni mia moja sabini za kitanzania.
Wafanyabiashara maarufu Harbinder Sing Sethi na James Rugemalira wanaohusishwa na kashfa ya ufisadi ya Tegeta Escrow wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi.
Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Harry Kitilya, pamoja na maafisa wa benki ya Stanbic mlimbwende wa taifa wa zamani (Miss) wa Tanzania Shose Sinare na Sioi Sumari pia wanakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi.
Wengine waliopo mahabusu kwa mashtaka kama hayo ni viongozi wa kitaifa wa mpira wa miguu, bwana Jamal Malinzi na Michael Wambura ambao ni rais na makamu wa raisi wa zamani wa Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF).

Comments