Kwa nini wapiganaji wa Majimaji wameamua kuweka silaha chini DR Congo?

Wapiganaji nchini DR Congo
Wapiganaji wa kundi la Maimai nchini Congo, wameitikia wito uliotolewa na rais wa nchi hiyo Felix Tshisekedi, wa kuweka chini silaha na kujiunga na jeshi la serikali au kurudi katika maisha ya kawaida.
Mamia ya wapiganaji hao kutoka kundi la UPCL wamejikusanya katika mji mdogo wa Kalunguta tayari kwa kusalimisha silaha zao.
Kulingana na meya wa mji wa Beni Bwanakawa Masumbuko Nyonyi aliyezungumza na BBC, hatua hiyo inatokana na wito wa rais wa taifa hilo Felix Tshisekedi wa kuwataka wapiganaji hao kuweka chini silaha mwezi wa Aprili mwaka huu
Kulingana na meya huyo wito huo unatokana na mateso waliopitia wakaazi wa mji huo na viunga vyake mbali na mipango ya kuimarisha jeshi la taifa hilo ili kuweza kukabiliana na wapiganaji wa ADF ambao wametajwa kuwa maadui wakubwa wa serikali ya taifa hilo.
''Tangu rais wa DR Congo alipopita mjini Beni alitoa wito kwa wapiganaji wa Majimaji kuweka chini silaha kutokana na mateso walioyapitia wakaazi wa mji huo kufuatia uvamizi wa mara kwa mara wa wanamgambo wa ADF, baadhi yao wamekubali wito huo'', alisema.
Hatahivyo amesema kwamba ni kundi dogo la wapiganaji hao ambalo limekubali kuweka silaha chini ili kujumuishwa katika ujenzi wa taifa hilo ambalo baadhi ya maeneo yake yamekuwa yakikabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa kipindi cha muda mrefu.
Huku akitoa wito kwa makundi mengine katika mji wa Beni kuiga mfano huo, Bwanakawa amesema kuwa baadhi ya wale waliokubali kuweka chini silaha watajumuishwa kwenye jeshi mbali na huduma nyengine za kitaifa huku wale wanaotaka kupelekwa nyumbani pia wakihudumiwa na kusafirishwa hadi makwao.
''Kila mtu ataulizwa aina ya kazi anayotaka kufanya au kujifunza iwapo ni ujasusi atapelekwa huko na kuna wale ambao watafunzwa kazi za mkono - kama huduma ya taifa. Kuna njia nyingi ambazo wakati watachukuliwa wataingizwa ili waridhike''.
Meya wa Beni Bwanakawa NyonyiHaki miliki ya pichaBWANAKWA /FACEBOOK
Aidha amesema kwamba wapiganaji walio na umri mdogo walioshinikizwa kujiunga na jeshi kama vile watoto wadogo watawasiliushwa katika mashirika yasiokuwa ya kiserikali ili kusaidiwa na baadaye kurudishwa nyumbani.
''Tunajua kwamba wanamgambo wa majimaji hawakuwa wakifuata sheria za kimataifa kwamba hawafai kuwapatia watoto silaha, hivyobasi kuna watoto walio na umri wa hata miaka 15 waliopatiwa silaha ili kujumuika katika vita, kitu tutakachofanya ni kuwachukua na kuwakabidhi mashirika yasiokuwa ya kiserikali ili kuwasaidia kabla ya kuwarudhisha nyumbani kwao''.
Meya huyo amesema kwamba jitihada za serikali ya DR Congo ni kuhakikisha kuwa wanasalia na adui mmoja ambaye ni wapiganai wa ADF.

Makubaliano

Alipoulizwa iwapo kuna mkataba au makubaliano yoyote yalioafikiwa kati ya serikali na wanamgambo hao , meya huyo alisema kwamba hakuna mkataba wowote uliowekwa isipokuwa kwamaba rais wa taifa hilo aliona mateso yanayowakabli wakaazi wa mji huo na kutoa wito huo. Hatahivyo amseama kwamba mkataba unaoweza kuafikiwa ni ule wa kurudisha amani katika mji huo na maeneo ya kandakando na jinsi ya kukabiliana na wanamgambo wa ADS kwa pamoja.

Usalama

Amesema kwamba hatua hiyo ya kundi la UPLC itapiga jeki mipango ya jeshi la FDRC kupambana na wanamgambo sugu wa ADF.
''Wakati jeshi la FDRC linapojipanga kukabiliana na ADS halafu linasikia wanamgambo wa majimaji wamejitokeza inakuwa vigumu wao kuendelea na vita hivyo kwa kuwa watalazimika kurudi nyuma na kuanza kuwakabili wapiganaji wa majimaji lakini iwapo wapiganaji wa maji maji wataweka silaha zao chini na kujiunga na FDRC nguvu zetu zitaelekezwa kwa ADF''.
Aliongezea kwamba iwapo eneo hilo litakuwa na amani maafisa wa afya vilevile watafanikiwa kupigana na ugonjwa wa Ebola kwa kuwa kwa sasa wapiganaji hao wa majimaji hawaruhusu maafisa wa afya kukabiliana na ugonjwa huo baada ya saa moja usiku.

Je huo utakuwa mwisho wa kundi hilo?

Meya huyo wa mji wa Beni amesema kwamba hiyo haitakuwa mara ya kwanza kwa Wapiganaji wa Majimaji kukubali kuweka silaha chini halafu baadaye kuamua kurudi porini.
''Tumekuwa tukiwauliza kwa nini munarudi porini baada ya kukubali kuweka silaha chini na jibu lao limekuwa ndugu zao na dada zao wanachinjwa na ADS bila kupata msaada wowote kutoka upande fulani. Sasa tunafikiri kwamba kesho hawatapata sababu nyengine ya kurudi porini. Tutahakikisha kuwa sehemu za Beni zinakuwa na usalama''.

Comments