Kampuni za mafuta za Total na Tullow zashindwa kuafikiana biashara

Ujenzi wa bomba la kusafirishia mafuta kutoka Uganda mpaka bandari ya Tanga Tanzania umesitishwa.
Hatua hiyo, kwa mujibu wa mashirika ya habari ya kimataifa ya Reuters na Bloomberg ni kufuatia kampuni ya uchimbaji mafuta ya Tullow kushindwa kuwauzia kampuni za Total ya Ufaransa na CNOOC ya Uchina vitalu vya mafuta wiki iliyopita.
Kampuni ya Total ndiyo inasimamia ujenzi wa bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,445.
Tayari hatua za awali kuelekea ujenzi huo kama ramani, baadhi ya kandarasi na utanuzi wa bandari ya Tanga Tanzania zilishaanza.
"Shughuli zote za ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (East African Crude Oil Pipeline) ikiwemo kandarasi zimesitishwa mpaka hapo taarifa mpya itakapotolewa kutokana na kushindikana kwa mauzo ya visima," afisaa mmoja nchini Uganda ameiambia Reuters kwa sharti la kutotajwa jina.
Makubaliano ya uuzwaji wa vitalu hivyo yalivunjika Agosti 29 kutokana na mzozo wa kodi na mamlaka za Uganda.
"Kuvunjika kwa makubaliano ya mauzo kunaleta suitafahamu juu ya nani atagharamikia kitu gani katika kuendeleza mradi huo, ambao ungekuwa na mfumo sawia wa umiliki kama ule wa vitalu vya mafuta," kwa mujibu wa afisa huyo.
rAMANI
Image captionKampuni ya Total ndiyo inasimamia ujenzi wa bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,445.
Uganda iligundua mafuta ghafi miaka 13 iliyopita, lakini uchimbaji wa kibiashara ulicheleweshwa kutokana na kutokuwepo kwa miundombinu, ikiwemo bomba la mafuta.
Mradi wa ujenzi wa bomba hilo ulipangiwa kugharimu dola bilioni 2.5, kutoka Hoima. magharibi mwa Uganda mpaka bahari ya Hindi, Bandari ya Tanga Kaskazini mwa Tanzania.
Njia ya kupitisha bomba hilo ilikuwa ni moja ya masuala yaliyogonga vichwa vya viongozi wa Afrika Mashariki mwaka 2016.
Awali ilitazamiwa bomba hilo lingepitia nchini Kenya na kuishia kwenye bandari ya Lamu, kabla ya serikali ya Rais John Pombe Magufuli kutupa karata yake mezani.
Baada ya vishindo na vita ya chini kwa chini, Uganda iliamua kupitisha mafuta hayo nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Bloomberg, kampuni ya Total imegoma kutoa kauli yeyote juu ya usitishwaji wa ujenzi.

Yoweri Museveni kuzuru Tanzania

Museveni na MagufuliHaki miliki ya pichaIKULU, TANZANIA
Image captionRais Yoweri Museveni anatarajiwa kuingia Tanzania leo Alhamisi Septemba 5.
Wakati huo huo, Raisi wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni anatarajiwa kuwasili nchini Tanzania leo Alhamisi jioni.
Kwa mujibu wa ratiba rasmi iliyotolewa na serikali ya Tanzania, Museveni anatarajiwa kuzindua jengo la Taasisi ya Mwalimu Nyerere kesho Ijumaa.
Siku ya Jumamosi Museveni na Magufuli wanatarajiwa kuhudhuria kongamano la kwanza la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uganda.
Bila shaka usitishwaji wa ujenzi wa bomba hilo utakuwa ni moja ya mambo ambayo Magufuli na Museveni watayaongea katika vikao vyao vya faragha na pia si ajabu jambo hilo likajitokeza kwenye kongamano Jumamosi.

Comments