Na Baraka Lusajo-Rukwa
Mkuu mkoa
wa Rukwa Joachim Wangabo ameitaka mamlaka ya maji safi Sumbawanga SUWASA kumaliza changamoto ya maji katika miji midogo ya halmashauri zote za mkoa huo kwa kukaa na Wataalamu wa
Wizara husika na kuandaa utaratibu ambao
utasaidia wananchi kuondokana na adha ya ukosefu wa huduma ya maji.
Ameyasema hayo alipotembelea mradi
wa uboreshaji wa huduma ya maji safi unaoendelea kujengwa katika mji mdogo wa
Namanyere ili kujionea maendeleo ya mradi huo pamoja na kujua changamoto
zinazoukabili na hatimae kuona namna ya kuupatia ufumbuzi huku akiwa ameambata
na kamati ya ulinzi na Usalama ya mkoa pamoja na wataalamu wengine kutoka ofisi
ya mkuu wa mkoa wa Rukwa.
Amesema kuwa awali wananchi
waliaminishwa kuwa baada ya upanuzi wa bwawa la mfili shida ya maji ingekuwa
imekwisha, lakini matokeo yake baada ya upanuzi huo bado shida ya maji
imeendelea kuwepo ambapo sasa kuna mradi wa ujenzi wa matenki mapya ambayo
hayatakidhi mahitaji ya maji katika mji huo unaokuwa kwa kasi na hivyo kuwataka
kujipanga kumaliza tatizo hilo.
“Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha
Mapinduzi inasema huku kwenye miji mikuu ya wilaya inatakiwa kupata maji kwa
asilimia 85, ninyi mtatoa asilimia 46, sasa SUWASA mkae na Wataalamu wa Wizara
husika ya Maji muandae utaratibu ukae tayari tayari juu ya namna gani ya kuweza
kukimbiza huu mradi, watu wamechoshwa na subiri subiri hata waswahili wanasema
ngoja ngoja yaumiza matumbo,” Alisisitiza.
Awali akisoma taarifa ya mradi huo
meneja wa SUWASA Mhandisi Gibon Nzowa alisema kuwa shida inayosababisha mradi
huo kutofikia asilimia 85 ya upatikanaji wa maji katika mji huo ni kutokana na
kutokuwepo kwa mtandao wa kuyasambaza maji hayo kwa kilomita 15 lakini maji
yalipo katika chanzo yanatosheleza kwa asilimia 85 endapo tatizo la mtandao
litatuliwa na kisha kueleza shughuli za mradi huo.
“Kazi zinazotekelezwa ni ununuzi na
ufungaji wa pampu mbili za kusukumia maji, ulazaji wa bomba kuu kutoka bwawa la
mfili hadi kwenye tenki takriban kilomita 3.7, pia ujenzi wa tenki la lita
500,000 ambalo limeinuliwa kwa mita 12 ili kuwezesha maeneo mengi ya Namanyere
kupata maji, ulazaji wa mtandao wa usambazaji maji kwa kilomita 6.5, vile vile
katika mradi huu kutakuwa na dira za maji za kuunganishia wateja,” Alimalizia
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Nkasi Mh. Said Mtanda wakati akielezea hatua walizochukua kupambana kumaliza
tatizo hilo la upatikanaji wa maji katika mji wa Namanyere alisema kuwa kama
wilaya walikaa na kuandika andiko na kuhitaji Shilingi Bilioni 2.5 na
kuliwasilisha wizarani ambapo fedha hiyo ilipunguzwa hadi kufikia shilingi
Bilioni 1.5 hali iliyopunguza asilimia ya upatikanaji wa maji katika mji huo.
“Tulitafuta wataalamu wakaandika huu
mradi, wakaleta kwangu tukapitia tukaona ni mradi wa Shilingi bilioni 2.5
ambayo hiyo ingetuwezesha kusambaza maji maeneo yote yenye upungufu wa maji
katika mji wetu, kwahiyo Waziri alipokuja tulimkabidhi akasema tuwape SUWASA
nao baada ya kuipiti walipeleka wizarani ambapo wakapunguza kiwango cha fedha,
huu mradi ulikuwa ni wa Bilioni 1.8 lakini Mheshimiwa waziri akasema ipungue
hadi kufikia shilingi bilioni 1.5 lakini kama ingekuwa ule mradi wetu wa
Shilingi bilioni 2.5 tungekuwa na mtandao wa kilomita 15 kuliko huu wa sasa wa
kilomita 6,” alisema.
Mradi huo wa uboreshaji wa huduma ya
maji safi katika mji wa Namanyere unatarajiwa kumalizika mwezi Mei mwaka 2020
na kugharimu shilingi Bilioni 1.58 fedha zinazotolewa na serikali huku
ukitarajiwa kuhifadhi maji kutoka lita 350,000 hadi lita 850,000 na kufikia
asilimia 46 ya uaptikanaji wa maji katika mji huo.
Comments
Post a Comment