Na Ibrahim Yasini –Songwe.
WANANCHI wa vijiji vilivyopo kaya ya Mkwajuni
makao makuu ya wilaya Songwe mkoani Songwe,wameiomba serikali kuharakisha
ujenzi wa miradi ya maji kwenye kata na wilaya kwa ujumla inayosuasua
kukamilika kwake licha ya serikali kutoa Bil.1.6.
Wilaya ya Songwe ni moja ya wilaya mpya mkoani
Songwe iliyomegwa kutoka wilaya ya Chunya mkoani Mbeya miaka minne
iliyopita,inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu maji safi na salama
inayosababisha watu kuugua homa ya kipindupindu kwa kunywa maji machafu ya mito
na madimbwi.
Anna Kasole,mkazi wa Mkwajuni jana alisema
serikali imepiga marufuku matumizi ya maji ya Madimbwi na ya mito ikiwemo mto
Lulongo kutokana na madai kuwa maji hayo yanavimelea vya kipindupindu na kusema
bado hawajawaonesha maji mbadala ya kutumia.
Getruda Pulumbu,mkazi wa mkajuni,alisema
wamekuwa na kilio kikubwa juu ya ukosefu wa maji safi,lakini viongozi wa
serikali na wa kisiasa wameuwa wakiwatoa hofu kuwa changamoto hiyo nitaondolewa
lakini inaonekana kama ni ndoto kuondolewa.
Alisema mikutano mingi imefanyika ikitolewa
pia ahadi nyingi za kuondoa tatizo hilo ambalo pia hata wakandarasi wa mradi
waliletwa wakitangaziwa kuwa ndani ya miezi 6 watakamilisha ujenzi lakini hadi
sasa bado ni kitendawili.
Juma Sambo,mkazi wa Mkwajuni,alisema siku za
hivi karibuni katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na mbunge wa jimbo
hilo,walitangaziwa kuwa fedha zimetolewa tena za kimkakati zitakazoondoa tatizo
la maji lakini hali ni tete.
Alisema kutokana na kunywa maji yasiyo
salama,yamesababisha mamia ya watu kuugua kipindupindu kati ya hao 9 walifariki
dunia,na sasa bado baadhi ya watu wanaendelea kutumia maji ya kwenyemito na
madimbwi licha ya katazo kwa kuwa hawana sehemu mbadala ya kuchota.
Alfred Masuke,mganga mkuu wilayani humo,alisema
kuwa watu 9 wamefariki dunia mwaka 2017-18 kwa kuugua homa ya kipindupindu na
kuwa kwa sasa wamepiga marufuku matumizi ya maji ya mito lakini baadhi ya watu
wanakaidi katazo hilo.
Kumekuwa na kawaida ya watu hasa kipindi ncha
masika kufukua mchanga kwenye madimbwi na mito wakisaka maji na maji hayo
yamepimwa na kubainika yanavimelea vya kipindupindu.
Abraham Sambila,mwenyekiti wa halmashauri ya
wilaya hiyo,licha ya kukiri kuwepo na changamoto hiyo,alisema walipokea fedha
Bilioni 1.6 kwa ajili yamiradi ya maji lakini mkandarasi wa kampuni ya Fabec
Investment aliyepewa tenda ya miradi hiyo anasuasua kukamilisha.
Alisema kutokana na hali hiyo,walimuandikia
barua mbili za onyo na endapo hata kamilisha watamuandikia barua ya tatu ambayo
ni ya kuvunja mkataba,hivyo aliwaomba wanannchi wawe watulivu kwani ifikapo
Mwezi septemba mwaka huu miradi yote itakamilika.
Fillipo Mulugo,mbunge wa jimbo hilo,alisema ni
kweli miradi hiyo imechelewa licha ya yeye kumuangukia katibu mkuu wizara ya
maji kuomba fedha za kimkakati,lakini alisema walipomhoji mkandarasi alisema
atakamilisha miradi hiyo ndani ya miezi 2 kuanzia sasa.
Kukamilika kwa mradi huo kutatatua kero ya
maji ya muda mrefu,na wananchi pia wataondokana na hofu ya kuugua homa za
magonjwa ya milipuko kikiwemo kipindupindu kilichoua watu 9 kufa na kadhaa
kuugua.
Mwisho.
Comments
Post a Comment