Na Ibrahim Yassin,Songwe.
MADIWANI na watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Songwe mkoani Songwe kupitia kikao chao cha baraza wamekiri kupokea kiasi cha milioni 90 kutoka kwa kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Shanta Mine kwa ajili ya mchango wa maendeleo katika mwaka wa fedha 2019-2020.
Abdallah Mgonja,kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo,mwishoni mwa wiki,alisema wamepokea fedha hizo katika mpango wa kampuni hiyo kupitia ASSR na fedha hizo zitatumika kusaidia ujenzi wa kituo cha afya Totoe pamoja na ujenzi wa jengo litakalotumika kama soko la kuuzia madini.
Alisema baada ya agizo la Rais Dkt,John Magufuli la kutaka kila wilaya yenye fursa ya uchimbaji wa madini ihakikishe inajenga soko hivyo na wao wamepokea agizo hilo na tayari jengo lipo asilimia 90 na kwamba baada ya miezi miwili ijayo anauhakika soko hilo litaanza kutumika.
Alisema serikali inania njema na agizo hilo hivyo endapo wachimbaji wa madini wataanza kuuza kwenye soko hilo,serikali itakusanya mapato ya uhakika ukilinganisha na awali ambapo wachimbaji hao walikuwa wakienda kuuza madini hayo mikoa ya mbali ikiwemo Dar es salaam.
Hata hivyo,mkurugenzi huyo,alisema mbali na kampuni hiyo kusaidia kiasi hicho cha fedha,pia kampuni nyingine ya shane shine ilitoa magari aina ya Malori 10 yaliyotumika kubebea mchanga na tofali kupeleka kwenye maeneo ya miradi na kuifanya miradi hiyo ijengwe kwa haraka.
Hayo yalibainika wakati wa kikao cha baraza la madiwani kilichokaliwa kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo mwishoni mwa wiki,ambapo mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Abraham Sambila,mbali na kuyapongeza makampuni yaliyojitokeza kusaidia alisema madiwani na watendaji wanapaswa kuifuatilia miradi ili ikamilike kwa wakati.
Awali,akitoa salamu za wilaya,mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo,Samweli Jeremiah alisema wamejipanga kuhakikisha agizo la Rais linatimizwa na kwamba tayari soko la madini litaanza kufanya kazi ndani ya miezi miwili ijayo.
Alisema mbali na soko hilo,pia wamejipanga kuhakikisha fedha zilizotolewa na wadau kusaidia ujenzi wa miradi zinatumika kama ilivyokusudiwa na kwamba aliwaomba wadau wengine waone umuhimu wa kusaidia miradi ya maendeleo kuunga juhudi za wananchi za kujenga miradi.
Isaya Ndolomi diwani wa kata ya Gua (CCM) alisema wao kama madiwani kwa kushirikiana na watendaji wanauhakika watasimamia vyema miradi hiyo ili kujenga imani na wadau ya kuendelea kutoa michango pale inapohitajika.
Mwisho.
Comments
Post a Comment